Viwanja vinane nchini Tanzania vitafanyiwa ukarabati mkubwa baada ya kuorodheshwa kama vitatumika kwa ajili ya mazoezi katika Fainali za Mataifa ya Afrika AFCON 2027 katika ombi la pamoja la nchi za Afrika Mashariki ‘EAC’.
Leo Jumanne (Mei 23) ndio siku ya mwisho kwa nchi zinazotaka kuwa wenyeji kuwasilisha maombi yao kwa Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, huku Tanzania, Kenya na Uganda wakitarajia kuwasilisha ombi la pamoja kutaka kuandaa fainali hizo.
Wenyeji wa Kenya, Uganda na Tanzania wameshirikiana wakijaribu kuzileta fainali hizo za 36 za AFCON katika nchi hizo za Afrika Mashariki.
Katika ombi lao la pamoja, nchi tatu zilikubaliana kuwasilisha viwanja vitatu kila moja kwa ajili ya kuandaa mechi za fainali hizo.
Kenya imewasilisha Uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Moi (MISC), Kasarani (30,000), Uwanja wa Taifa wa Nyayo jijini hapa na ule wa Kipchoge Keino uliopo Eldoret.
Kama viwanja vya mazoezi, Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Nick Mwendwa amesema Nairobi itakuwa na viwanja vya MISC Kasarani Annex, Police Sacco, Klabu ya Michezo ya Chuo cha Utalii Kenya, Ulinzi Sports Complex na Jamhuri Sports Complex.
Kwa upande wa Uwanja wa Kipchoge Keino, kiongozi huo wa FKF alisema kuna viwanja vitatu vya mazoezi lakini hakuvitaja. Mwendwa alibainisha hayo wakati akizungumza na televisheni ya K24.
Endapo ombi la pamoja na EAC litapita, basi viwanja vinane kwa Kenya vinatarajia kufanyiwa ukarabati mkubwa tangu Shirikisho la Soka la Afrika ‘CAF’ kusema vinatakiwa kuwa vya hadhi ya kidunia.
Viwanja hivyo vinatakiwa kuwa na sehemu bora ya kuchezea pamoja na vyoo na vyumba vya kubadilishia nguo.
Mwendwa anaamini kuwa nchi hizo tatu zina nafasi kubwa ya kupewa nafasi ya kuandaa fainali hizo.
“Afrika Mashariki haijawahi kuandaa fainali hizo za Afcon, hivyo kwangu Algeria na Misri zenyewe zitakuwa zikisubiri kuandaa kama Afrika Mashariki itashindwa. Hawawezi kutupita kama sisi tutakuwa imara,” amesema Mwendwa