Mkazi wa Nzega mkoani Tabora, Mohamed Mashaka (29) amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita kwa kosa la kutumia kompyuta na kujitambulisha kuwa ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Akisoma hati ya mashtaka, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Scola Teffe ameiambia Mahakama kuwa bila uhalali kisheria, Mohamed alitumia njia ya mtandao kujitambulisha kuwa yeye ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Wakili Teefe amesema upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kuiomba Mahakama kupanga siku ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Mshatakiwa ambaye ni mwendesha mitambo katika mgodi wa Dhahabu Geita (GGML) anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 24, 2023 kinyume na Sheria ya mtandao namba 14 ya mwaka 2015 kifungu cha 15 (1 na 2).
Mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, Cleofas Waane, mshtakiwa amedaiwa kutenda kosa hilo akiwa maeneo ya mgodi wa GGM wilayani Geita.
Shauri hilo lmeahirishwa hadi Juni 8, 2023 itakapokuja tena kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.
Mshatakiwa ameachiwa kwa dhamna baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kusaini hati ya dhamana ya Sh5 milioni.