Mahakama Kuu nchini Kenya jana ilimhukumu adhabu ya kifo afisa mwandamizi wa Jeshi la polisi, Nahashon Mutua kwa kosa la kumuua mahabusu.
Uamuzi huo wa mahakama umetolewa baada ya kumkuta Mutua na hatia ya kumpiga na nondo mtuhumiwa Martin Koome hadi kufa, katika selo za polisi mwaka 2013.
Mutua alikuwa mkuu wa kituo cha polisi cha Nairobi wakati ambapo Koome alishikiliwa kwa tuhuma za kumpiga mkewe.
Kwa mujibu wa hukumu ya mahakama ilitolewa kwa waandishi wa habari, baada ya tukio hilo Mutua alijaribu kuficha ukweli kwa kutafuta sababu za visingizio lakini upelelezi ulimuumbua.
Juhudi za wanaharakati, makundi ya kutetea haki za binadamu pamoja, shinikizo kutoka kwa umma mitandaoni na kazi iliyofanywa na Taasisi Huru ya Kuangazia Polisi (Ipoa) vimetajwa kuwa sehemu ya sababu za haki hiyo kupatikana.
Kwa mujibu wa BBC, kazi za Ipoa ambayo ni taasisi ya kiraia zimeonekana kuzaa matunda zaidi nchini humo baada ya kuonekana maafisa wa polisi wakichukuliwa hatua mara kadhaa kwa makosa wanayofanya dhidi ya raia.
Katika kesi nyingine, maafisa watano wa jeshi la polisi wamekutwa na hatia katika kesi iliyokuwa ikiwakabili ya kumpiga na kitu kizito kichwani mtoto mwenye umri wa miezi sita, Samantha Pendo wakati wa vurugu za uchaguzi mwaka 2017 na kumsababishia kifo. Mtoto huyo alipoteza maisha akiwa anapatiwa matibabu hospitalini.
Mahakama imemtaka mwendesha mashtaka wa Serikali kuwahoji maafisa wengine 31 ambao wanaweza kuwa sehemu ya chanzo cha kifo cha mtoto Samantha Pendo.