Rais wa Senegal na Umoja wa Afrika, Macky Sall, amesema kuwa Bara la Afrika ni lazima lijifunze kujilisha badala ya kutegemea misaada ya chakula toka Mataifa wahisani.
Sall, ameyasema hayo katika mkutano wa ufunguzi wa The Dakar 2 Summit on Feeding Africa Food Sovereignty and Resilience, wakati akiwakaribisha viongozi wakuu wa nchi za Kenya, Nigeria, Tanzania, Zimbabwe, Mauritania na Zambia.
Amesema, “Ili kubadilisha uwezo wetu kuwa uhalisia, tunahitaji kutenga angalau 10% ya bajeti ya taifa kwa sekta ya kilimo”, Sall aliuambia mkutano huo uliojumuisha wakuu kadhaa wa nchi za Afrika.
Mkutano huo wenye kaulimbiu ya ‘Lisha Afrika Uhuru wa Chakula na Ustahimilivu’, ulioandaliwa kwa pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB ulibainisha kuwa baadhi ya Waafrika milioni 283 wana njaa kwani bara hilo ni makazi ya theluthi moja ya watu milioni 850 wanaokabiliwa na njaa duniani.
“Mkutano wa Dakar II utahamasisha dhamira ya kisiasa, mshirika wa maendeleo na uwekezaji wa sekta binafsi, kuanzisha sera zinazohitajika sana na kusukuma kimkakati hatua za kutekeleza kwa kiwango kikubwa tukio hili la kihistoria litakuwa hatua ya mabadiliko kuelekea uhuru wa chakula na ustahimilivu kwa bara zima”.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Kenya William Ruto alitoa wito wa kuchukuliwa hatua zaidi akisema bara Afrika limekuwa nyuma kwa muda mrefu sana.
Amesema, “Niseme ukweli kwamba tunafanya mazungumzo haya wengi wetu, kama wakuu wa nchi, kutoka bara letu, na tunajadili chakula, sio jambo la kupendeza sana. Nadhani tunapaswa kujadili zaidi ya chakula miaka 60 baada ya uhuru.”
Mkutano huo wa kilele wa siku tatu, unaofanyika huko Diamniadio karibu na Dakar mji mkuu wa Senegal unamalizika Ijumaa, Januari 27.