Katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani hii leo Juni 2023. Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wananchi kutambua wajibu walionao wa kutunza vyanzo vya maji, kuacha mazoea ya kutupa taka hovyo na kuagiza kila kaya kuwa na sehemu mahsusi ya kuhifadhia ama kuchomea taka.
Dkt. Mpango ameyasema hayo Juni 5, 2023 jijini Dodoma na kuongeza kuwa, masuala ya kufanya usafi na utunzaji mazingira hayana mbadala kwa kuwa mazingira ndio uhai na yana mahusiano ya moja kwa moja na ustawi wa Taifa kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jafo amesema suala la utunzaji na uhifadhi wa mazingira limeendelea kupewa kipaumbele hapa nchini ambapo kwa kutumia Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kauli mbiu iliopo ni yenye lengo la kuhamasisha ajenda ya utunzaji wa mazingira na kutunza vyanzo vya maji.
Aidha, amewapongeza wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu kwa kujitoa kihifadhi mazingira ikiwemo kampeni ya soma na mti yenye lengo la kuhamasisha upandaji wa miti mashuleni. na kuwashukuru wadau mbalimbali katika jitihada zao za kuhakikisha suala la mazingira linapewa kipaumbele kwa maendeleo endelevu.