Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amewasilisha maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanzania Women CEOs Roundtable la kuitaka TWCR kushirikiana na Baraza la Taifa la Biashara – TNBC, ili kubaini maeneo yenye uhitaji.
Ushirikiano huo, unalenga kuandaa programu za kujenga uwezo, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Watoto na Makundi Maalum iimarishe kanzidata ya Viongozi na Maafisa Watendaji Wakuu Wanawake katika Sekta ya Umma pamoja na Sekta Binafsi.
Amesema, Bodi hiyo na Taasisi za Sekta Binafsi ziangalie namna ya kujenga uwezo kwa wataalam wabobezi wanawake katika uendeshaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya Kitaifa, kutengeneza mikakati itakayoleta matokeo chanya katika ustawi wa wanawake na Taifa kwa ujumla.
“Imarisheni huduma za uwezeshaji katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na makundi ili kupunguza umaskini na Utoaji na tuzo na vyeti kwa Maafisa Watendaji Wakuu Wanawake wanaofanya vizuri kwenye Taasisi na sekta mbalimbali ni jambo la msingi katika kuhamasisha ushiriki wa wanawake wengi kwenye shughuli za kuchumi nchini,” amesema Katambi.
Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Jukwaa la Maafisa Watendaji Wakuu Wanawake Tanzania – TWCR, Emma Kawawa ametoa wito kwa wanawake kuwa wajasiri, kujiamini na kuthubutu katika kuanzisha Biashara ili kujikomboa kiuchumi.