Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Katavi imempandisha kizimbani Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira wa Manispaa ya Mpanda (MUWASA), Hussein Salumu Nyemba.
Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi, Stuart Kiondo amesema Nyemba amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda akiwa na mtuhumiwa mwingine Kaimu Afisa Utumishi wa MUWASA, Justine Wambali mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda, Gaspher Luoga.
Watuhumiwa hao, walisomewa mashitaka mawili kila mmoja ambapo shitaka la kwanza ni la kutumia vibaya madaraka na pili kuisababishia MUWASA hasara ya shilingi 17,817,000 kinyume na sheria ya uhujumi uchumi sura ya 200 iliyorejewa mwaka 2022.
Amesema, Desemba 12, 2022 Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa akiwa Manispaa ya Mpanda alitoa maagizo kwa TAKUKURU kumfanyia uchunguzi Mkurugenzi huyo na mwenzake ambapo wamebaini watuhumiwa hao wote wawili wanahusika juu, ya tuhuma hizo.
Aidha, Kiondo amesema maagizo ya Waziri Mkuu yalilenga kumfanyia uchunguzi Hussein Nyemba, lakini Justine Wambali amejumuishwa kwenye kesi hiyo kwa nafasi yake ambapo alishindwa kumshauri mkurugenzi wake na kuajiri watumishi 37 bila kufuata utaratibu na kuisababishia MUWASA hasara ya kiasi hicho cha fedha .
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alifanikiwa kutimiza masharti ya kuwa nje kwa dhamana, huku mtuhumiwa Justine Wambali akiendelea kuhangaikia taratibu za dhamana na hadi muda wa kuhairishwa kwa kesi alikuwa bado hajafanikiwa.