Chama cha Soka nchini Zambia ‘FAZ’ kimemtangaza Kocha wa zamani wa Klabu ya Chelsea Avram Grant kuwa Mkuu wa Benchi la Ufundi la Timu ya Taifa ya Nchi hiyo ‘Chipolopolo’.
Grant ametangazwa kushika hatamu, akichukua nafasi ya Aljosa Asanovic Raia wa Croatia aliyedumu kazini tangu Januari 2022, akilitumikia Taifa hilo katika michezo 11, akishinda minne, sare miwili na kupoteza mitano.
Kocha huyo kutoka nchini Israel amesaini mkataba wa miaka miwili, ambao una kipengele cha kuhakikisha Zambia inashiriki Fainali za ‘AFCON 2023’ zitakazopigwa nchini Ivory Coast.
Mshahara wa Kocha huyo ambaye pia aliwahi kupita kwenye klabu ya West Ham United ya England, kwa mwezi atalipwa Dola za Marekani 25,000 sawa na Shilingi za Tanzania Milioni 58.3
Kazi ya kwanza kwa Kocha Grant itakuwa katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za ‘AFCON 2023’ dhidi ya Lesotho, utakaopigwa mjini Lusaka Mwezi Machi 2023.
Baadae mwezi huo Zambia itacheza mchezo mwingine ugenini dhidi ya Lesotho kabla ya kuivaa Ivory Coast, kisha Comoro mwezi Setpemba.