Baada ya kutangazwa kuwa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Simba SC, Ahmed Ally amefunguka kwa mara ya kwanza akiwa visiwani Zanzibar.
Ahmed alitangazwa kuchukua nafasi ya ukuu wa idara hiyo leo Jumatatu (Januari 03) Asubihi, kupitia kurasa za mitandao ya kijamii za Simba SC, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Haji Manara na baadae kushikwa kwa muda na Ezekiel Kamwaga.
Ahmed amesema ameipokea kwa mikono miwili nafasi hiyo na anaamini ataitendea haki, kutokana na taaluma ya habari aliyonayo.
Amesema lengo lake kubwa ni kutumika kama daraja la kufikisha habari kutoka kwa Uongozi wa Simba SC kwenda kwa Mashabiki na Wanachama, hivyo atafuata weledi kwa kutimiza majukumu yake ipasavyo.
“Nimeipokea nafasi hii kwa uzito wa Dunia Nzima, ni habari njema, ni habari kubwa, ni habari nzuri kweli kweli, ni ndoto imetimia ya kwenda kufanya kazi ndani ya Simba SC, kwa hiyo uzito wa habari hii unaweza kusema ni uzito wa Dunia Nzima.”
“Naimani mimi ni chaguo sahihi kwa klabu ya Simba na ndio maana mchakato wa kumtangaza Afisa Habari wa Simba SC ulikua mrefu, hii ilimaanisha Uongozi ulikua unafuta mtu sahihi na mkweli na awe Simba SC.” amesema Ahamed
Tayari Ahmed Ally ameshaanza kazi yake ndani ya Simba SC kwa kusafiri na kikosi hadi kisiwani Zanzibar kwa ajili ya kutoa habari za klabu hiyo wakati wote wa michuano ya kombe la Mapinduzi 2022 iliyoanza rasmi jana Jumapili (Januari 02).
kabla ya kutangazwa kuwa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Simba SC, Ahmed Ally alikua akihudumu kama Mwandishi na Mtangazaji wa Azam Media, Pia aliwahi kufanya kazi Sahaha Media Group inayomiliki vituo vya Radio Free Africa na Star TV.