Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally ameitisha Azam FC kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao utapigwa baadae leo Alhamis (Oktoba 27), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Ahmed amesema Simba SC ipo tayari na imara kuelekea mchezo huo, ambao watakua ugenini licha ya kuhamishwa Uwanja kutoka Azam Complex-Chamazi, ambako ulipaswa kuchezwa kabla ya mabadiliko yaliyotangazwa mapema Jumatatu (Oktoba 24).
Amesema wanatambua wanakwenda kukutana na timu ya aina gani, lakini haitawazuia kuwapelekea ‘Pumzi ya Moto’ na kuondoka na alama tatu muhimu.
“Unaona tumetoka kulazimisha sare na watani zetu wa jadi, sasa tunakwenda kukutana na Azam FC, tutawapelekea ‘Pumzi ya Moto’ hata wao wanalifahamu hili.”
“Kwanza wametoka kumtimua Kocha, hapo unaona namna gani tutakuwa na nguvu ya kuwakabili, tunawaheshimu lakini tunazitaka alama tatu.”
“Tumejiandaa kushinda mchezo wetu dhidi ya Azam FC, lakini sio mchezo huu tu, bali tunataka kuhakikisha tunashinda mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar, kama ambavyo yalikua malengo yetu mwezi huu Oktoba, ambao tunakabiliwa na ratiba ngumu” amesema Ahmed Ally
Simba SC ambayo tayari imeshashuka dimbani kwenye michezo sita za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23, imekusanya alama 14, ikishinda michezo minne na kutoka sare miwili.