Kikosi cha Simba SC leo Alhamis (Mei 05) kitaanza maandalizi ya mchezo wa Mzunguuko wa 23 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting utakaopigwa Jumapili (Mei 08), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Simba SC iliwasili jijini Dar es salaam jana Jumatano (Mei 09) ikitokea Lindi kupitia mkoani Mtwara baada ya kumaliza mchezo wake dhidi ya Namungo FC juzi Jumanne (Mei 03), na kuambulia matokeo ya sare ya 2-2.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally amesema baada ya kuwasili jijini Dar es salaam, wachezaji wote wa Simba SC walipewa mapumziko kwa ajili ya kusheherekea sikukuu ya Eid El Fitri, na leo Alhamis (Mei 05), watarejea kambini kuendelea na mpango wa kuikabili Ruvu Shooting Jumapili (Mei 08).
“Kikosi baada ya kurejea jana Jumatano, Benchi la Ufundi liliwapa ruhusa wachezaji kuungana na familia zao ili kumalizia sherehe za sikuku ya Eid El Fitri, na leo Alhamis wataanza maandalizi ya mchezo unaofuta.” amesema Ahmed
Kuhusu mpango wa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, Ahmed Ally amesema Simba SC bado haijakata tamaa na itaendelea kupambana hadi mwisho, kwa kuamini michezo iliyosalia lolote linaweza kutokea.
“Kama timu kubwa tunawajibika kufanya jitihada za kupambana hadi mwisho, Simba hata ikicheza michezo ya kirafiki ni lazima ipate ushindi, ikipoteza huo mchezo ama ikipata sare katika huo mchezo, Mashabiki, Wanachama na wachezaji wanaumia, kwa hiyo hakuna kilichopungua zaidi ya kuendeleza mapambano hadi kieleweke.”
“Jambo lingine ambalo linaendelea kutupa msukumo wa kupambana ni kuwafurahisha Mashabiki na Wanachama wetu ambao wanahitaji kufurahi wakati wote, ukishinda kila mmoja ndani ya Simba anafurahi, hivyo bado tuna jukumu la kuhakikisha tunashinda michezo yetu, halafu mambo mengine tutaangalia baadae.”
“Isifike mahala ukakosa ubingwa na vile vile ukaumiza mioyo ya Mashabiki na Wanachama wa Simba SC, jukumu zito hapa ni kuhakikisha tunashinda michezo yetu kwa lengo la kuendelea kutetea kilichopo mikononi mwetu halafu kuwafurahisha Mashabiki na Wanachama wetu.” amesema Ahmed Ally.
Simba SC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 42, ikiachwa na Young Africans kwa alama 13, baada ya Wananchi kushikwa shati jana Jumatano (Mei 05) Uwanja wa Lake Tanganyika dhidi ya Ruvu Shooting.