Mabalozi 42 wa Tanzania kutoka nchi mbalimbali Duniani wamesema kuwa ujenzi wa mradi wa Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3) umekuja wakati muafaka, ambapo wawekezaji wengi wanapenda kwenda nchi zenye miundombinu bora naya kisasa.
Mabalozi hao wametoa kauli hiyo leo walipofanya ziara ya Kikazi ya kutembelea Jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3).
Balozi Wilson Masilingi anayeiwakilisha Tanzania nchini Marekani, amesema kuwa jengo hilo ni la kisasa na lina vifaa bora, ambapo Watanzania wanapaswa kujivunia maendeleo haya, ambapo sasa kuna mpango wa safari za kutoka moja kwa moja kutoka Tanzania hadi Marekani.
Naye Balozi Abdallah Possi anayeiwakilisha Tanzania nchini Ujerumani, amesema kuwa jengo hilo sasa litachagiza uwingi wa watalii kutoka nchi mbalimbali duniani, ambapo ndege nyingi zitatumia JNIA.
”Miradi hii ukiwemo huu wa jengo la tatu la abiria ni muhimu kwa wageni wanaoingia nchini, kwani litarahisisha usafiri kwa watu wa Mataifa mbalimbali wanaoingia nchini na kutoka, amesema Dkt. Possi.
Balozi Fatma Mohamed Rajabu anayewakilisha nchi nchini Qatar, amesema anatarajia ongezeko la ndege ya Air Qatar kwa safari za Tanzania, pamoja na kuja kila siku mara moja.
“Nitaenda kueleza ubora wa jengo letu hili na ninaimani pamoja na ndege ya Qatar inakuja kila siku lakini wanaweza kuongeza safari kwani tumekuwa na jengo la kisasa zaidi na lenye kupokea abiria wengi,” amesema Balozi Fatma.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dkt. Wibroad Slaa ametoa wito kwa Mabalozi wenzake kuitangaza zaidi Tanzania Kimataifa kwa kuonyesha miradi yote mikubwa na uwekezaji wanaoweza kuwekeza sehemu mbalimbali nchini.
“Msiogope kulitangaza Taifa letu katika maendeleo yanayofanyika sasa chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuweza kuwekeza kwa ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati,”amesema Dkt. Slaa.
Hata hivyo, mabalozi hao wamesifu juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano iliyopo chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale amesema kuwa jengo hilo linauwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka, ambapo lina vifaa vya kisasa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Julius Ndyamukama amesema jengo hilo pia lina ukumbi wa Wafanyabiashara Mashuhuri.