Karibu watu 40 wamefariki Dunia na wengine 78 kujeruhiwa baada ya kutokea kwa ajali ya basi nchini Senegal ambapo Rais Macky Sall amesema ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Ginvy, eneo la Kaffrine majira ya saa tisa na nusu alfajiri.
Tukio hilo, lilihusisha mabasi mawili ambayo yaligongana huku Rais wa Senegal, Macky Sall aki tweet kwa kuandika, “Nimehuzunishwa sana na ajali mbaya ya barabarani ya leo (Jumapili Januari 8, 2023), huko Gniby. Ninatuma rambirambi zangu za dhati kwa familia za wahasiriwa na ninawatakia majeruhi ahueni ya haraka.”
Mara baada ya andiko hilo, Rais Sall pia ametangaza siku tatu za maombolezo kuanzia leo Jumatatu Januari 9, 2023, huku akiitisha mkutano wa mawaziri wa Serikali yake kujadili hatua za usalama barabarani na katika ajali hiyo watu 78 walijeruhiwa huku baadhi yao wakipata majeraha makubwa.
Mwendesha mashitaka wa Serikali, Cheikh Dieng amesema ajali hiyo ilitokea baada ya basi la umma kupasuka tairi na kupoteza mwelekeo kabla ya kuligonga basi jingine lililokuwa likitokea upande wa pili na kupelekea kutokea kwa mkasa huo.