Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameweka jiwe la Msingi la mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya wasichana ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, iliyopo Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma ambayo itapokea wanafunzi 1,080 mara baada ya kukamilika kwake.

Ujenzi huo, unatekelezwa kwa awamu mbili kwa gharama ya shilingi bilioni 4 kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), awamu ya kwanza ilianza April 2022 na ikitarajiwa kukamilika Januari 30, 2023 kwa shilingi bilioni 3 ambapo wanafunzi 600 watapokewa kwa awamu ya kwanza.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Awamu hiyo ya kwanza imehusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo mabweni matano, bwalo, vyumba 12 vya madarasa, jengo la utawala, nyumba ya mwalimu, mfumo wa maji safi na maji taka, vyoo matundu 16, uzio, kichomea taka, chumba cha jenereta na njia za kutembelea.

Aidha, awamu ya pili ambayo ujenzi wake unatarajiwa kuanza ndani ya mwaka huu kwa gharama ya shilingi bilioni moja itahusisha ujenzi wa madarasa 10 yenye ofisi za walimu tatu, chumba cha ICT, Maktaba, nyumba nne za walimu na mabweni manne.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua maendeleo ya Ujenzi katika hospitali ya Wilayani Namtumbo akiwa katika ziara Mkoani Ruvuma.

Waziri Mkuu, pia amewataka wakandarasi wanaojenga shule hiyo kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo kwa muda uliopangwa ili waanze kupokea wanafunzi. Shule ya Sekondari Dkt. Samia Suluhu Hassan inatarajia kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano Julai, 2023.

Marekani wampata Spika wa Bunge kwa mbinde
Mtoto wa miaka 6 ampiga sisasi Mwalimu wake