Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Nassredine Nabi ameanza kuifuatilia Al Hilal ya Sudan ili kufanikisha mpango wa klabu hiyo katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Young Africans imejiwekea malengo ya kucheza hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23, na tayari imeshatinga hatua ya Kwanza ya Michuano hiyo, baada ya kuifunga Zalan FC ya Sudan Kusini jumla ya mabao 9-0.
Kocha Nabi amesema baada ya kupata uhakika wa kikosi chake kucheza dhidi ya Al Hilal ya Sudan, ameanza kufuatilia kwa ukaribu mipango na mikakati ya klabu hiyo ambayo ina historia kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Amesema Al Hilal ni klabu kubwa na nguli katika Michuano ya Kimataifa, inajua namna ya kupambana na kufikia malengo iliyojiwekea, hivyo hana budi kupambana kikamilifu kukiandaa kikosi chake kwa kuzingatia atakachokipata kwenye uchunguzi wake dhidi ya wapinzani hao kutoka Sudan.
“Al Hilal ni timu nzuri yenye wachezaji wazuri na Kocha mzoefu (Florent Ibenge) hivyo ili uweze kupata ushindi dhidi yao unatakiwa kuwaangalia kwa jicho la tatu, kitu ambacho nimeanda kukifanyia kazi tangu walipocheza na St George ugenini na kisha mchezo wao wa juzi walipocheza nyumbani kwao Sudan,”
“Tunaendelea kukusanya video za michezo yao waliyocheza siku za karibuni na kabla hatujarudi kambini kesho Jumatano (Septemba 21) kuanza maandalizi yetu tutakua tumekamilisha hili, ili kuanza kuwapa mbinu wachezaji wetu.” amesema Kocha Nabi
Young Africans itaanzia nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kukipiga na Al Hilal ya Sudan kati ya Oktoba 07-09, na juma moja baadae itakwenda Omdurman-Sudan kucheza mkondo wa pili kati ya Oktoba 14-16.