Aliyekuwa makamu wa Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ambaye Rais Robert Mugabe alimuondoa kwenye nafasi hiyo wiki hii ameripotiwa kukimbia nchi hiyo kwa madai ya kuhofia usalama wake.
Rais Mugabe alimtangaza Mnangagwa kuwa ni adui wa Serikali yake akidai kuwa alikuwa anapanga njama za kushika dola.
“Alienda kwa nabii kanisani ili aambiwe Mugabe atakufa lini. Lakini aliambiwa angekufa yeye kwanza,” Mugabe aliwaambia waandishi wa habari Jumatano alipotangaza kumtumbua Mnangagwa.
Rais Mugabe aliongeza kuwa walikuwa wakifuatilia mienendo yake kwa muda mrefu na njama alizokuwa akipanga kushika dola bila kufuata utaratibu wa chama na kwamba wameona wamuondoe yeye lakini wale aliokuwa akishirikiana nao watajua namna ya kuishi nao wakiwa ndani ya chama cha ZANU-PF.
Mke wa Rais Mugabe, Grace Mugabe anatajwa zaidi kuwa ndiye atayechukua nafasi ya Makamu wa Rais huku ikielezwa kuwa ni sehemu ya kumtengenezea njia ya kurithi nafasi ya mumewe.
Mama Grace amekuwa na uadui mkubwa na Mnangagwa akimtaja kuwa ni msaliti. Pia, alimfananisha na nyoka ambaye alidai anapaswa kuondolewa mapema.
Hata hivyo, tamko lililotolewa na watu wa karibu wa Mnangagwa limekanusha kuwa alikuwa na njama zozote dhidi ya Serikali hiyo na kwamba amekuwa mwaminifu wakati wote kwa Rais Mugabe.