Klabu ya Fulham imemsajili mlinda mlango kutoka nchini Ufaransa Alphonse Areola, akitokea kwa mabingwa wa League 1 Paris St-Germain.
Areola mwenye umri wa miaka 27, amejiunga na miamba hiyo ya magharibi kwa London kwa mkopo wa muda mrefu, na anaaminika atapeleka changamoto kwenye nafasi ya ulinzi wa lango.
Msimu uliopita Paris St-Germain walimtoa kwa mkopo mlinda mlango huyo kwa mabingwa wa Hispania Real Madrid, ambapo alicheza michezo minane pekee, ikiwepo michezo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA).
“Nimefurahishwa na hatua ya kujiunga na klabu hii,” amesema Areola.
“Meneja Scott Parker alizungumza nami mara kadhaa, alinishawishi kuja hapa.”
“Fulham ni klabu yenye historia kubwa hapa London, nimesikia mengi mazuri kuhusu klabu hii, ninatarajia kufanya makubwa nikiwa hapa.”
Kwa upande wa muwekezaji mwenza wa klabu ya Fulham Tony Khan, amekiri kufurahishwa na usajili wa mlinda mlango huyo ambapo amesema: “Alphonse ana uzoefu wa kutosha, ana kila sababu ya kuwa hapa.”
“Amecheza timu ya taifa ya Ufaransa, ametwaa ubingwa wa Ufaransa akiwa na PSG, amepata mafanikio akiwa na RC Lens, Bastia, Villarreal na Real Madrid, sababu hizo ndizo tunajivunia sana kwa kumsajili mlinda mlango huyu.”
Mlinda mlango huyo mwenye urefu wa futi 6 na inchi 5, ameshaitumikia timu ya taifa ya Ufaransa mara tatu, na alikua sehemu ya kikosi kilichotwaa ubingwa wa kombe la dunia mwaka 2018.