Mshambuliaji wa Klabu ya Chelsea, Alvaro Morata ameachana rasmi na timu hiyo na kujiunga na Atletico Madrid kwa mkopo, hadi mwishoni mwa msimu wa mwaka 2019/20.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alijiunga na The Blues Julai 2017 akitokea Real Madrid, akiweka rekodi nzito wakati huo ya kitita cha £60 milioni. Alimwaga wino wa kuitumikia timu hiyo kwa miaka mitano.
Akiwa na Chelsea, ameshiriki katika michezo 47 akipachika jumla ya magoli 16. Ikumbukwe kuwa Atletico Madrid ndiyo klabu iliyomkuza Morata kabla ya kuanza kupata nguvu na kukipiga Real Madrid.
Tayari ameshaanza kukamilisha mchakato wa kutua rasmi uwanjani kuitumikia Atletico Madrid, akitarajiwa kufanyiwa vipimo nchini Hispania, Jumapili hii.
Morata anapishana na mshambuliaji kutoka nchini Argentina, Gonzalo Higuain aliyejiunga na Chelsea wiki iliyopita.
Mara ya mwisho kuonekana uwanjani akiitumikia Chelsea ni Januari 5 mwaka huu, wakati timu hiyo ilipokipiga dhidi ya Nottingham Forest na kujipatia ushindi wa 2-0.
“Nina furaha sana kuwa hapa [Atletico Madrid] na ninajivunia. Nasubiri kwa hamu kuanza mazoezi, kukutana na wachezaji wenzangu wapya,” alisema Morata.
Kupitia tovuti yao, Atletico Madrid wameandika, “Morata amethibitisha uwezo wake kama mfungaji mzuri katika baadhi ya mechi za Ulaya zenye ushindani mkubwa zaidi.”