Mwenyekiti wa klabu ya Stand Utd, Aman Vincent amemtuhumu rais wa shirikisho la soka nchini TFF, Jamal Emil Malinzi kwa kumjumuisha katika sakata la sintofahamu ya uongozi linayoendelea mkoani Shinyanga.

Vincent anayedaiwa kusimamishwa uanachama na baadhi ya wanachama wa Stand Utd kupitia mkutano mkuu wa hadhara ulioendeshwa na mkuu wa wilaya ya Shinyanga mjini mwanzoni mwa mwezi huu, amesema Malinzi hawezi kukwepa lawama katika sakata la mgogo linaloendelea kwa sasa.

Kiongozi huyo ambaye alikua mstari wa mbele kuingoza Stand Utd tangu walipokua ligi daraja la kwanza kabla ya kupanda na kucheza ligi kuu msimu wa 2014-15, amesema kulikua na haja kwa rais wa TFF kulitolea ufafanuzi wa kina sakata linaloendelea, lakini ameamua kukaa kimya huku akijua taratibu za soka zinavyoagiza.

“Malinzi anahusika katika hili, yeye ndio mkuu wa mamlaka ya soka Tanzania na anapaswa kuzungumza na vyombo vya habari na kueleza mustakabali wa Stand Utd ambaye ni mwanachama wa TFF,”

“Haiwezekani suala hili kuendelea kuchukua nafasi kila siku katika vyombo vya habari na tayari kuna barua kadhaa zilizoelekezwa kwenye ofisi za TFF, ila Malinzi ameendelea kukaa kimya.” alisema Aman Vincent

Hata hivyo Vincent amesisitiza kutohofia jambo lolote kwa sasa na badala yake ameamua kusema ukweli wa mambo kwa kumuhisha rais wa TFF katika sakata linaloendelea.

Amesema huenda ufafanuzi unashindwa kutolewa na TFF kwa makusudi ya kuwategea baadhi ya watu kuzungumza ukweli ambao huenda ukawatia majaribuni na kufikia hatua ya kufungiwa na kamati za shirikisho hilo.

“Sina budi kusema ukweli wa jambo hili, na niwaambie kwamba mimi simuogopi mtu kwa kuhofia kufungiwa, kwanza nina umri mdogo, nina miaka 34 hivyo ikitokea wananijadili na kunifungia nitafanya shughuli nyingine za kimaisha, lakini nitakua nimesema ukweli kuhusu mazingira ya soka la nchi hii yanavyoendeshwa na rais Malinzi wa TFF.”

“Haiwezekani mkuu wa wilaya ya shinganya mjini anaingilia masuala ya soka na kufanya maamuzi yaliyo kinyume na katiba, mtu kama Malinzi anayejua sharia na kanuni za soka, anakaa kimya na kuangalia kinachoendelea Stand Utd.” Aliongeza Amani Vincent

Kuhusu uchaguzi wa viongozi Aman Vincent alishindwa kuzungumza jambo lolote na badala yake aliagiza jambo hilo kuelekezwa kwenye kamati ya uchaguzi ambayo wameiunda wao kama viongozi wa Stand Utd kampuni huku wakitarajia uchaguzi mkuu kufanyika Juni 24.

Mbali na uchaguzi huo, pia kamati ya muda ya uongozi wa Stand Utd, nayo imeandaa inaendelea na mchakato wa uchaguzi mkuu ambao umepangwa kufanyika Juni 26 mwaka huu.

Antonio Conte Ajipanga Kuwahamisha Candreva, Bonucci
Mwakyembe kuliburuza mahakamani gazeti la 'Dira' kwa kuandika ametapeli bilioni 2