Waziri wa Katiba na Sheria, Dk.Harrison Mwakyembe amesema kuwa atalishtaki mahakamani gazeti la Dira ya Mtanzania kwa kuandika habari inayomhusisha na utapeli wa shilingi bilioni 2.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mwakyembe ambaye amekanusha vikali habari hizo zilizoandikwa na Dira ya Mtanzania toleo la Juni 13 mwaka huu, amesema kuwa gazeti hilo limeonesha dhahiri kuwa limekosa ueledi na limepotosha kwa kiasi kikubwa.

“Nikiri kuwa sijawahi kushuhudia upotoshaji mkubwa na wa makusudi kama huu. Ukiisoma taarifa za gazeti hili utaona waziwazi umakini na weledi wa uandishi wa habari unakosekana, hata jina la wizara yangu limekosewa,” alisema Mwakyembe.

Dk. Mwakyembe ameweka wazi kuwa yeye na wakili wake wamepanga kufungua kesi mahakamani wakiangalia pia athari za kuhusishwa kwa vituo vya runinga vya ITV na Star TV.

“Tutafungua kesi hii mahakama kuu ya Tanzania na bado mimi na mawakili wangu tunaangalia impact na kuhusika kwa vyombo vikubwa vya  habari  kama ITV na Star Tv  kwa kutangaza taarifa,” alisema Dk. Mkwakyembe.

Alisema kuwa gazeti hilo limekuwa likiandika habari za upotoshaji akitoa mfano wa habari iliyoeleza kuwa kifaru cha kivita cha Jeshi la Wananchi kiliibwa na wanakijiji, habari ambayo amesema inalitia doa jeshi hilo. Waziri Mwakyembe alisema kuwa gazeti hilo haliwezi kuvuliwa kwa mwenendo huo.

Gazeti la Dira ya Mtanzania ambalo hutoka kila Jumatatu, limekuwa likiandika habari za kiuchunguzi ambazo mara nyingi huwa mada kuu ya siku kwenye mitandao. Juni 13 mwaka huu liliandika habari yenye kichwa cha habari ‘Mwakyembe atuhumiwa kutapeli bilioni 2, kupandishwa mahakamani wakati wowote’.

Aman Vincent: Malinzi Anahusika Katika Mgogoro Wa Stand Utd
Chelsea, Arsenal Kumuwania Alvaro Morata