Matukio ya mashambulizi ya anga na makombora, yameendelea katika mji mkuu wa Sudan Khartoum baada ya pande mbili zinazovutana kushindwa kukubaliana kusitisha mapigano.
Pande hizo mbili za Jeshi rasmi la Serikali na wanamgambo wa RSF wameshindwa kukubaliana kusitisha mapigano licha ya kuahidi kuwalinda raia na kuruhusu kupisha misaada ya kibinadamu.
Tamko la kanuni za makubaliano llisainiwa mjini Jeddah nchini Saudi Arabia, baada ya mazungumzo ya takriban wiki moja kati ya pande hizo mbili, ingawa hakuna upande hata mmoja ambao mpaka sasa umetoa taarifa ya kuyatambuwa makubaliano hayo.
Makubaliano hayo, yametokana na mazungumzo yaliyosimamiwa na Saudi Arabia na Marekani na yanajumuisha ahadi za pande zote mbili kuruhusu raia, wataalamu wa afya, misaada ya kibinadamu pamoja na kupunguza madhara kwa raia na majengo ya umma.