Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amekitaka Chama Cha Mawakili Tanganyika – TLS, na Kamati ya Mawakili kuchukua hatua kali dhidi ya mawakili wanaoharibu heshima ya taaluma ya sheria kwa kukosa uadilifu.

Dkt. Mpango ameyasema hayo hii leo Mei 11, 2023 wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa TLS uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha – AICC, na kukemea tabia ya baadhi ya mawakili kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa na kuharibu kesi.

Amesema, “kumekuwa na tuhuma za baadhi ya mawakili kujihusisha na vitendo vya rushwa na udanganyifu kwa maslahi yao binafsi ikiwemo kuwasaliti wateja kwa kupokea rushwa kutoka upande wa pili.”

Aidha, Dkt. Mpango ameongeza kuwa, TLS inatakiwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria kutoa elimu kwa umma kuhusu suala la mihuri ya kielektroniki ili kuondokana na suala la vishoka na mawakili wanaotumia mihuri isiyo halali kufanya kazi za uwakili.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro amewataka wanachama wa TLS kushiriki kikamilifu katika mchakato wa katiba mpya, pamoja na ule wa mabadiliko ya sheria zinazohusiana na Siasa, Uchaguzi na Demokrasia.

Uimarishaji mazingira wezeshi kwa wawekezaji unaendela - Jafo
Rais Dkt. Mwinyi apokea ripoti ya CAG