Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linamshikilia Mwanamke mmoja anayefahamika kwa jina la Estaroda Kaduma (28) mkazi wa Kichiwa kwa tuhuma za kumuua Mtoto wa Kaka yake baada ya kumfafanisha na Ng’ombe.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe Hamis Issah amesema kijana huyo anayefahamika kwa jina la Brown James Kaduma (7) aliyekuwa anasoma darasa la kwanza katika Shule ya msingi Kichiwa alikuwa amelala majira ya saa nane usiku wakati Shangazi yake akiwa anafanya maombi.

Amesema wakati maombi yakiendelea shangazi alianza kupambana kwa kumpiga Mtoto akidhani ni ng’ombe mkubwa mweusi aliyefika wakati akifanya maombi.

“Huyu Dada huwa ana tabia ya kufanya maombi na katika maombi yake akaona ng’ombe mkubwa mweusi amefika katika eneo ambalo anafanya maombi, akaacha maombi akaanza kumpiga huyo ng’ombe na baadaye akatoweka baada ya muda akaonekana amefariki Kijana mdogo Mtoto wa Kaka yake baada ya kukanyagwakanyagwa kichwani na kujeruhiwa sehemu nyingine za mwili,” amesema Kamanda Issah.

Kamanda Issah amesema tukio hilo linahusishwa na imani za kishirikina na kutoa wito kwa Wananchi kuachana na imani hizo ambazo zimekuwa zikileta madhara makubwa kwenye jamii.

Madaktari waanza uchunguzi mshukiwa wa Ebola
Wahanga wa Ugaidi kupewa kipaumbele huduma za jamii