Mfanyabiashara, Hamis Said (38), anayekabiliwa na kesi ya kumuua mkewe, Naomi Marijani, leo Agosti 27 ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumpatia laini zake mbili za simu zenye zaidi ya Shilingi Milioni 5 ili azitoe pesa hizo kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kwake na ada ya mwanaye.
Mshtakiwa ametoa ombi hilo mbele ya Hakimu Mkazi, Salum Ally kwa madai ya kwamba anazo simu nne zinazoshikiliwa katika kituo cha Polisi cha Central na kwamba laini mbili kati ya hizo zina shilingi milioni 5, na kuomba laini hizo apatiwe hata ndugu yake akatoe pesa na ikiwezekana zitolewe na polisi wakiwepo.
Aidha, kabla ya maelezo hayo, Wakili wa Serikali Wankyo Simon ameieleza mahakama kuwa shauri hilo lilifika mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa, ambapo upelelezi bado haujakamilika na kuomba kesi iahirishwe na kupangiwa tarehe nyingine.
Baada ya kueleza hayo, Wakili Wankyo ameeleza kuwa simu hizo ni sehemu ya upelelezi, hivyo kwa sasa ni ngumu kumpatia kwasababu hawawezi kuamini moja kwa moja kama kweli anahitaji kutoa pesa, na ukizingatia kesi inayomkabili ni ya mauaji, hivyo amemshauri kama anahitaji pesa zake aandike barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 10, 2019.
Ikumbukwe kuwa Hamis Said anakabiliwa na kosa la mauaji ambalo anadaiwa kulitenda Mei 15,2019, eneo la Geza Ulole Kigamboni jijini Dar es Salaam, ambapo inadaiwa alimuua mke wake na kisha kuuchoma mwili wake kwa kutumia magunia mawili ya mkaa na kuyafukia mabaki ya mwili wake shambani.