Meneja wa klabu ya Olympique de Marseille inayoshiriki Ligue 1 nchini Ufaransa, Andre Villas-Boas amesema kufuatia kifo cha mchezaji nguli ulimwenguni Diego Maradona, Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA linapaswa kuistaafisha jezi namba 10 kwa timu zote duniani.
Maradona alifariki dunia jana Jumatano (Novemba 25) akiwa na umri wa miaka 60, huku taarifa za kifo chake zimethibitishwa na Shirikisho la soka nchini Argentina kupitia kwa Rais wake Claudio Tapia.
Boas amesema amesikitishwa na taarifa za kufariki dunia kwa gwiji huyo aliewahi kutamba katika medani ya soka kati ya mwaka 1976-1994 akiwa na timu ya taifa ya Argentina, pamoja na baadhi ya klabu za soka Barani Ulaya na Amerika ya kusini.
“Ni taarifa mbaya, ningependa FIFA kuistaafisha jezi namba 10 kwenye michuano yote na kwa timu zote, itakuwa ni heshima kubwa sana kwake.’’ Amesema Boas.
Hata hivyo klabu ya soka ya SSC Napoli aliyowahi kuitumikia gwiji huyo, iliacha kutumia jezi namba 10 kwenye michezo yake yote tangu mwaka 2000 ikiwa ni ishara ya kumpa heshima mchezaji huyo ambaye alikuwa ni mmoja ya waliosaidia klabu hiyo kutwaa mataji 2 ya Ligi Kuu ya Italia ‘Serie A’ pindi alipokuwa akiitumikia.
Klabu nyingine ambazo Maradona aliwahi kuzitumikia ni Argentinos Juniors (1976–1981, 1995–1997), Boca Juniors (1981–1982), FC Barcelona (1982–1984), SSC Napoli (1984–1991), Sevilla CF (1992–1993) na Newell’s Old Boys (1993–1994).
Klabu alizowahi kuzifundisha kama kocha ni Deportivo Mandiyú (1994), Racing Club (1995), Al-Wasl (2011–2012), Deportivo Riestra *Kocha msaidizi* (2013–2017), Fujairah (2017–2018), Dorados de Sinaloa (2018–2019) na Gimnasia de La Plata (2019–2020).
Kwa upande wa timu ya taifa Maradona aliifundisha timu ya taifa ya wakubwa ya Argentina (2008–2010), ambayo aliitumikia kama mchezaji kuanzia 1977–1994 , akitangulia kuitumikia timu ya taifa ya taifa hilo chini ya umri wa miaka 20 kuanzia mwaka 1977–1979.