Imefahamika kuwa mshambuliaji kinda wa FC Barcelona Ansu Fati, atakuwa nje ya uwanja kwa miezi minne baada ya kupata majeraha wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Real Betis.
Mchezo huo uliomalizika kwa FC Barcelona kuibuka na ushindi mnono wa mabao matano kwa mawili, ulishuhudia kinda huyo akitolewa nje ya uwanja wakati wa kipindi cha pili baada ya kuumia goti lake la mguu wa kushoto.
Taarifa rasmi kutoka FC Barcelona zimeeleza kuwa, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 18 amefanyiwa upasuaji kwa mafanikio jana jumatatu, Novemba 09.
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa, Fati huenda akarejea tena dimbani mapema mwezi Machi mwaka 2021.
“Mchezaji wa kikosi cha kwanza Ansu Fati, amefanyiwa upasuaji salama na Dr. Ramon Cugat kwenye goti lake la kushoto chini ya uangalizi wa wafanyakazi ya afya wa klabu. Fati atakuwa nje kwa takribani miezi minne, kuanzia leo Jumatatu (Novemba 09).”