Mshambuliaji wa pembeni wa klabu bingwa nchini Ujerumani (FC Bayern Munich) Arjen Robben, ametangaza kustaafu kuitumikia timu ya taifa ya Uholanzi baada ya kuifungia mabao mawili usiku wa kuamkia hii leo dhidi ya Sweden.
Robben alifunga mabao hayo katika uwanja wa Amsterdam ArenA, kwenye mchezo wa mwisho wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia hatua ya makundi barani Ulaya.
Hata hivyo ushindi huo wa mabao mawili kwa sifuri, haukuisaidia Uholanzi kufuzu fainali za kombe la dunia za 2018, huku wakiiacha Sweden ikipata nafasi ya kushiriki mchezo wa mtoano (play-off) ikitokea kundi A.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 33 amefikia maamuzi hayo, huku akiacha kumbukumbu ya kushiriki mashindano sita makubwa duniani, na kucheza michezo 96 ambayo imeshuhudia akifunga mabao 37 kwa kipindi cha miaka 14.
-
Trinidad na Tobago yaizima Marekani, ndoto za 2018 zayeyuka
-
Ureno, Ufaransa zafuzu Kombe la Dunia Marekani yatupwa nje
“Inatosha kwa sasa, ninaamini ni wakati mzuri kwangu kutangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa, ni zamu ya kizazi kipya ambacho kitakua na jukumu la kusaka mafanikio ya kucheza michuano mikubwa duniani na kutwaa mataji,” alisema Robben.
Robben ambaye alikua nahodha wa timu ya taifa ya Uholanzi, aliisaidia Uholanzi kufika hatua ya fainali ya kombe la dunia mwaka 2010 kabla ya kufungwa bao moja kwa sifuri dhidi ya Hispania, na mwaka 2014 alikua miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Uholanzi kumaliza katika nafasi ya tatu katika fainali za kombe la dunia kwa kuwafunga wenyeji Brazil.