Uongozi wa Klabu ya Arsenal umeripotiwa kufikia makubaliano na Beki wa kati kutoka Ufaransa William Saliba, huku ikitajwa amekubali kusaini mkataba mpya wa miaka minne.

Mpango huo wa Arsenal umechukua nafasi kubwa, ili kuhakikisha Beki huyo haondoki katika kipindi hiki ambacho klabu hiyo imedhamiria kukiboresha kikosi chake kuelekea msimu ujao, ambao wanaamini watarejea katika mapambano ya Ubingwa.

Saliba alikuwa kwenye ubora mkubwa kwenye timu ya Arsenal msimu wa 2022-23 na jambo hilo limefanya klabu kibao kuhitaji saini yake ikiwamo mabingwa wa soka wa Ufaransa, Paris Saint-Germain.

Pia beki huyo ameanza kuhusishwa na mpango wa kuwaniwa na Mabingwa wa Soka nchini England Manchester City.

Saliba aliumia mwezi Machi na kushindwa kuitumikia timu yake, lakini kabla ya kuumia alifunga mabao matatu na kuasisti mara moja katika mechi 33 na hakika aliunda kombinesheni matata kabisa na beki mwenzake Gabriel Magalhaes.

Meneja wa Arsenal Mikel Arteta alikuwa anahangaika kuhakikisha kwamba anamsainisha mkataba mpya beki huyo ili kuepuka kusumbuliwa na timu nyingine zitakazohitaji saini ya mchezaji huyo, na kwa mujibu wa taarifa kutoka jijini London, inaelezwa amefaikiwa.

Saliba angekuwa huru kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, lakini Januari mwaka huu Arsenal ilikifanyia kazi kipengele cha kumuongezea miezi 12 zaidi katika mkataba wake na hivyo mchezaji huyo mkataba wake utafika tamati majira ya kiangazi 2024.

Wema usiooza wamnufaisha Bibi mtoa msaada
Mashujaa: KMC, Mbeya City yoyote FRESH