Aliyekua meneja wa klabu ya Arsenal ya England Arsene Wenger, anaongoza katika kinyang’anyoro cha kuwania nafasi ya kocha mkuu wa timu ya taifa ya Japan.
Chama cha soka nchini Japan, kinaamini Wengewr ataweza kuifanya kazi yake vilivyo na kuipa mafanikio timu yao ya taifa, endapo wataafiki kumchukua, kutokana na kuwahi kufanya kazi nchini humo miaka ya 90 akiwa na klabu ya Nagoya Grampus Eight, kabla ya kutimkia nchini England kujiunga na Arsenal mwaka 1996.
Japan wapo katika mchakato wa kumsaka kocha mpya, baada ya kumtimua Vahid Halilhodzic, aliyefanikisha safari yao ya kushiriki fainali za kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi, miezi miwili kabla ya kuanza kwa fainali hizo.
Nafasi ya kocha huyo kutoka nchini Bosnian ilichikwa kwa muda wa kocha mzawa Akira Nishino, ambaye alifanikiwa kuifikisha Japan katika hatua ya 16 bora na kufungwa mabao matatu kwa mawili dhidi ya Ubelgiji.
Vahid Halilhodzic
Mkataba wa muda wa kocha huyo mzawa unatarajiwa kufikia kikomo mwishoni mwa mwezi huu, na uongozi wa FA ya Japan hauna budi kuendelea na mchakato wa kumsaka kocha mkuu wa kikosi cha timu ya taifa.
Akira Nishino
Wenger amewahi kuhusishwa na mipango ya kuajiriwa kwenye klabu za Real Madrid na Paris Saint-Germain, lakini hakufanikiwa kufuatia klabu hizo kupata mameneja ambao tayari wameshatangazwa kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Mbali na klabu hizo za barani Ulaya pia mzee huyo wa kifaransa amewahi kuhusishwa na taarifa za kuwani na klabu kadhaa za nchini China, tangu alipotangaa kuachana na Arsenal mwezi Mei.
Wenger hajawahi kufundisha soka katika ngazi ya timu za taifa, na kama atatangazwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Japan, itakua ni mara yake ya kwanza kufanya hivyo, baada ya kufanya kazi kama mkuu wa benchi la ufundi upande wa klabu.
Klabu zilizonolewa na babu huyo mwenye huyo mwenye umri wa miaka 68 ni Nancy 1984–1987, AS Monaco 1987–1994, Nagoya Grampus Eight 1995–1996, Arsenal 1996–2018.