Kikosi cha Young Africans mapema hii leo kilianza safari ya kuelekea mkoani Rukwa, mjini Sumbawanga, tayari kwa mchezo wa Kombe la Shirikisho (ASFC) utakaowakutanisha dhidi ya Maafande wa Tanzania Prisons mwishoni mwa juma hili.
Young Africans wameondoka jijini Dar es salaam, kwa ndege hadi jijini Mbeya kisha watatumia usafiri wa gari kuelekea mjini Sumbawanga, tayari kwa mchezo huo ambao utaunguruma siku ya Ijumaa (April 30).
Mabingwa hao wa kihistoria katika Soka la Bongo wamefanya safari ya kuelekea Nyanda za Juu Kusini, huku wakiwa na machungu ya kupoteza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC waliochomoza na ushindi wa bao moja kwa sifuri, siku ya jumapili (April 25), Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kocha Mkuu Mpya wa Young Africans Nasreen Al Nabi ni sehemu ya wasafiri walioelekea mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, ambapo mchezo dhidi ya Tanzania Prisons utakua wa pili kwake tangu alipokabidhiwa jukumu la kuwa mkuu wa benchi la ufundi klabuni hapo, akichukua nafasi ya Juma Mwambusi.
Kabla ya kuanza safari kocha huyo amesema hana hofu na mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu pamoja na Kombe la Shirikisho (ASFC), huku akisisitiza msema kweli ni hesabu za kuelekea mchezo wa mwisho msimu huu 2020/21.
“Kwa sasa kila mmoja anajipanga kupata ushindi ili kujiimarisha, huwezi kujua nini kitatokea katika mechi zilizobakia, hakuna ambaye ana uhakika na kile ambacho anakitaka, tutaendelea kujipanga kutafuta matokeo mazuri,” alisema Nabi.
Young Africans inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 57, ikitanguliwa na Simba SC yenye alama 58, huku Azam FC ikishika nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 54.