Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi, inamshikilia Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Likongowele, Mohamedi Ndope maarufu (Kifuku), kwa tuhuma za kupokea rushwa ya Sh 300,000.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa TAKUKURU mkoani Lindi, Noel Mseo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa Ndope amekamatwa katika eneo la Nangando, Liwale Mjini, Julai 28 mwaka huu saa 1:00 usiku.
Inadaiwa kuwa Ndope alimshawishi mtumishi wa Idara ya Afya Kata ya Likongowele akiomba rushwa hiyo ili aweze kumsaidia mtumishi mwenzake asichukuliwe hatua za kisheria kutokana na kile kilichoelezwa kuwepo kwa malalamiko dhidi ya mtoa taarifa kutoka kwa wananchi.
Akizungumzia kukamatwa kwa kiongozi huyo, Noel Mseo amesema Julai 28 mwaka huu walipokea taarifa kutoka kwa mtumishi wa Idara hiyo ya Afya kuwa aliombwa kutoka kwa Kiongozi huyo wa Chama cha Siasa kiasi cha Tsh 300,000/ ili aweze kumtetea asichukuliwe hatua za kinidhamu, kiasi ambacho alipewa.
“Baada ya mlalamikaji kuja Ofisini kwetu kumlalamikia huyu kiongozi, tulichukuwa hatua ikiwa ni pamoja na kuweka mtego tukafanikiwa kumtia mkononi akipokea fedha hiyo”, amesema Mseo.
Hata hivyo, Mseo ameongeza kuwa mtuhumiwa atafikishwa mahakamani muda wowote kujibu shitaka linalomkabili, mara baada ya kukamilika kwa mahojiano.