Wanajeshi 18 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamepandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza wakikabiliwa na kesi ya ubakaji wa halaiki wa watoto.
Wanajeshi hao wanadaiwa kuwabaka watoto wa kike 46 katika kijiji cha Kavumu na kwamba kati yao walikuwemo wenye umri hadi miezi 18 tu.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya mwaka 2013 na 2016 kwa sababu za imani ya kishirikina kuwa damu ya wasichana bikira ingeweza kuwapa nguvu ya ajabu na ulinzi.
Hata hivyo, kiongozi wa wanajeshi hao anayetambulika kwa jina la Frederic Batumike na wenzake walikana mashtaka hayo.
Makundi ya haki za binadamu yanaamini kuwa ufunguzi wa kesi hizo ulioanza wiki iliyopita utamaliza utamaduni wa ubakaji unaochukuliwa kama sehemu ya ‘nguvu ya kivita’ nchini humo.
“Kuanza kwa mashtaka haya ni ishara yenye nguvu kuhusu kuanza kwa vita dhidi ya ubakaji hasa wa watoto,” alisema Jean Chrysostome Kijana, mwanaharakati anayewawakilisha wahanga wa matukio hayo.
Wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu wameeleza kuwa matukio hayo yalikuwa magumu kufanyiwa uchunguzi kwani wahanga walikuwa na umri mdogo sana.