Askofu wa Kanisa la Good News For All Ministry, Dkt. Charles Gadi ameipongeza Serikali kwa kushirikiana bega kwa bega na familia za wafiwa na wananchi wa mkoa wa Arusha  katika kuomboleza  msiba uliotokana na ajali iliyosababisha vifo vya wanafunzi 32, waalimu wawili na dereva wa shule ya Lucky Vicent.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo jijini Dar es salaam, amesema kuwa Kanisa lake linaungana na famili za marehemu hao kuomboleza msiba huo mkubwa ulioacha simanzi kwa familia na taifa kwa ujumla.

Amesema kuwa Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli imefanya kazi kubwa kuwaunganisha wananchi wa mkoa wa Arusha na kuleta faraja kwa Watanzania na familia zilizopoteza watoto wao.

“Tunaipongeza Serikali yetu ya Rais Dkt. John Magufuli kwa jinsi ilivyouchukulia msiba huu kwa uzito mkubwa. Tumeguswa sana jinsi Makamu wa Rais Samia Suluhu alivyoshiriki kwenye kuaga miili ya watoto hao.” Amesema Askofu Gadi.

 

Hata hivyo, Katika hatua nyingine Askofu Gadi aliongoza maombi ya kumuomba Mungu mvua iache kunyesha mkoani Dar es Salaam na ukanda wa pwani badala yake Mungu aielekeze kwenye mikoa mingine ambako inahitajika kwa ajili ya kilimo na shughuli nyingine.

Serikali kujenga kivuko cha juu kawe bondeni
Video: Young Dee ashangazwa na tabia ya Profesa Jay, 'nimejifunza'