Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania – JWTZ, litasafirisha misaada iliyotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda nchi ya Malawi ambayo imeathiriwa na Kimbunga Freddy.
Akitoa ufafanuzi hii leo Machi 18, 2023 Jijini Dodoma, Msemaji wa JWTZ, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda amesema misaada hiyo inahusisha vyakula, mahema na misaada mingine ya kibinadamu.
Amesema, “kufuatia maafa ya kimbunga nchini Malawi, Serikali imeamua kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu ili kuisaidia nchi jirani, na JWTZ imepewa jukumu la kusafirisha misaada hiyo.”
“Tunatarajia shehena zitaondoka muda wowote kuanzia sasa, jumla ya tani 1,000 za unga wa mahindi zitasafirishwa kwenda Malawi, amesema tani 90 zitaondoka kila siku zikitokea Dodoma,” amesema.
Aidha, Luteni Kanali Ilonga ameongeza kuwa, “tani 60 za unga wa mahindi zitaondoka kila siku kutokea mkoani Iringa, mablanketi 6,000 yataondokea Dodoma, mahema yasiyopungua 50 yataondoka yakitokea jijini Dar es Salaam.”
Machi 13, 2023 Kimbunga kilichoambatana na mvua kubwa na upepo mkali kiliikumba nchi ya Malawi kiasi cha kutangazwa kuwa janga chini humo baada ya kusababisha Vifo vya watu zaidi ya 100 na kuharibu miundombinu, nyumba, mazao na athari zingine.