Mkuu wa Hospitali ya Arbaminch kusini mwa Ethiopia ameiambia BBC kwamba misumari 30, chuma na vitu vingine vimeondolewa kutoka kwenye tumbo la mfungwa mmoja wa Ethiopia.
Temesgen Teshome alisema mfungwa huyo alihukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani na kwa sasa anatibiwa ugonjwa wa akili.
Mtu huyo alilazwa katika Hospitali ya Arbaminch Jumanne iliyopita baada ya kupata maumivu ya tumbo na hali yake ilikuwa mbaya, kulingana na Teshome.
Madaktari walipomuuliza alikokuwa ameshikiliwa, alijibu kwamba alikuwa amemeza misumari.
Madaktari baadaye walipiga picha ya X-ray na kugundua kuwa tumbo lake na utumbo vilikuwa vimefunikwa na misumari na vipande vya chuma.
Kwa mujibu wa Temesgen Teshome, mfungwa huyo alifanyiwa upasuaji baada ya njia ya umeng’enyaji chakula kuzibwa kabisa.
”Wakati wa upasuaji, ilibainika kuwa vitu hivyo vilipenya kwenye tumbo na utumbo, hivyo upasuaji ulilazimika kufanyika kwa umakini,” alisema Teshome.
Karibu misumari 30, kalamu nne, sindano, uzi na vipande vya chuma viliondolewa kwenye tumbo lake.
Baada ya upasuaji, madaktari walipiga picha ya x-ray ya mtu huyo, kuthibitisha kama hakuna kitu kingine kilichoachwa ndani ya tumbo lake.
”Yuko kwenye hali nzuri. Anahitaji vipimo zaidi. Alimeza vitu hatari vyenye ncha. Inawezekana tumbo lake limeharibika.” alisema mkuu wa hospitali.
Aliongeza kuwa mfungwa huyo bado anahitaji uchunguzi wa kitabibu kutazama koo lake na uchunguzi wa wataalamu wa matatizo ya kiakili.
Maafisa wameiambia BBC kuwa mfungwa huyo awali hakuwa akihisiwa kuwa na ugonjwa wa akili, lakini alikuwa akihisi kuugua baada ya kukamatwa.