Mwanamke mmoja raia wa Uganda amejitokeza akitafuta haki kufuatia kugundulika kuwa hana Virusi Vya Ukimwi baada ya miaka sita ya kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo kutokana na kupimwa vibaya.
Faridah Kiconco mwenye umri wa miaka 37, alianza kutumia ARVs baada ya kipimo cha VVU alichofanya mwaka 2011 akiwa mjamzito kuonyesha ana virusi hivyo.
Akizungumza na Daily Monitor, Kiconco alisimulia kwamba alimeza dawa hizo bila kukosa ili kuokoa maisha yake, lakini mwaka wa 2017, baada ya kujifungua mtoto wake wa pili, alianza kuona mabadiliko fulani katika mwili wake.
Ngozi yake ilianza kugeuka manjano, na viungo vyake vya mwili vilianza kuwacha kufanya kazi vizuri na alirejea katika Kituo cha Afya cha Kabwohe IV, ambacho kilithibitisha kuwa ana VVU na kupimwa tena.
Baada ya kupata majibu hospitali hiyo ilimtuma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbarara (MRRH), ambako alithibitishwa kuwa hana VVU baada ya uchunguzi zaidi kufanyika, na sampuli zilipelekwa katika mji mkuu wa taifa hilo.
“Siku tatu baadaye, (Kituo cha IV cha Afya cha Kabwohe) kilinipigia simu na baada ya kusoma matokeo, aliniambia sina VVU,” Kiconco alisimulia.
Tangu wakati huo, alifungua kesi akitaka kulipwa fidia kwa uharibifu ambao ARVs zimemsababishia.
“ARVs ziliathiri viungo vyake vya mwili kama vile figo na ini. Tunataka alipwe fidia kwa madhara aliyoyapata kutokana na ARV,” wakili wake alisema.
Kinachosikitisha ni kwamba tangu 2018, kesi yake haijawahi kusikilizwa, lakini alisema hatakata tamaa katika kutafuta haki.