Kesi ya madai ya utakatishaji fedha inayomkabili Rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake, Godfrey Nyange ‘Kaburu’, imesomwa leo na kupelekwa mbele mpaka tarehe 22, machi 2018.
Kutokana na Evans Aveva ambaye ameripotiwa kuwa amelazwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU), Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), hali iliyopelekea kushindwa kuhudhuria mahakamani kusikiliza kesi hiyo inayomkabili.
Hayo yameelezwa leo Machi 8, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri na wakili anayewatetea, Evodius Mtawala wakati kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo.
”Mshatakiwa wa Kwanza Aveva tangu jana amelazwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi hali yake siyo nzuri” amesema Wakili Mtawala.
Hata hivyo mwendesha mashataka wa Takukuru Leonard Swai naye ameliambia mahakama kuwa Aveva ni mgonjwa na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Mtawala ameiambia mahakama kuwa walizungumza na upande wa mashtaka wataeleza jalada la kesi hiyo bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), na wameomba wapewe siku 14 ili waweze kueleza kitu .
Kwa mara ya kwanza Kesi hiyo ya madai ilitajwa Julai 20, 2017 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Aveva na Kaburu wanakabiliwa na tuhuma za kughushi nyaraka za Klabu ya Simba na kutakatisha dola 300,000 (zaidi ya Sh milioni 650) na wamekuwa rumande tangu Juni 29, mwaka 2017.