Benchi la ufundi la Azam FC limetoa tathmini ya michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara waliyocheza kanda ya Ziwa na kuambulia alama mbili baada ya kulazimishwa sare na Biashara United FC kisha Gwambina FC.
Jana, Jumatatu (Desemba 7) ikiwa Uwanja wa Gwambina Complex Azam FC ililazimisha sare ya bila kufungana na Gwambina FC na mchezo wake uliopita Uwanja wa Karume ililazimisha sare ya kufungana bao moja kwa moja dhidi ya Biashara United.
Azam FC imekua na matokeo mabaya kwa michezo kadhaa, hali iliyoufanya uongozi wa klabu hiyo kufanya mabadiliko kwenye benchi la ufundi kwa kusitisha mkataba wa kocha Mromania Aristica Cioaba, na kumuajiri kocha kutoka Zambia George Lwandanina.
Kocha msaidizi wa klabu hiyo yenye maskani yake Chamazi jijini Dar es salaam Vivier Bahati amesema, matokeo ambayo wameyapata kanda ya Ziwa kwenye michezo miwili hayakuwa mpango kazi wao hivyo watajipanga kufanya vizuri kwenye michezo ijayo.
Bahati amesema: “Huku kanda ya Ziwa mambo yamekuwa tofauti na vile ambavyo tulipanga kwa kukosa kupata matokeo chanya hivyo ni darasa kwetu.”
“Bado kuna michezo mingine mbele yetu hizo tutapambana kupata matokeo chanya ambayo yatatufanya turejee pale ambapo tulikuwa ndani ya uwanja.”
Azam FC walianza kwa kasi msimu wa 2020/21 kwa kushinda mfululizo michezo saba ya mwanzo na kujikusanyia alama 21.
Mambo yamewaendea hovyo kwenye michezo saba ya hivi karibuni ambapo wameshinda mchezo mmoja, sare tatu na kupoteza michezo mitatu na kujikusanyia alama sita walipokuwa wakisaka alama 21.
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Azam FC ipo nafasi ya pili ikiwa na alama 27 baada ya kucheza michezo 14, wakitanguliwa na Young Africans mwenye alama 34 baada ya kucheza michezo 14.