Uongozi wa Klabu ya Azam FC, umejinasibu kuwa kwenye mpango wa kutumia faida ya matokeo mabaya ya vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Young Africans, ili wakae juu yao.
Mpaka sasa, Azam FC ipo nyuma ya Young Africans kwa tofauti ya alama sita ambapo wababe hao wa Azam Complex Chamazi wamecheza michezo 24, huku Young Africans wakicheza michezo 23.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Azam FC Zakaria Thabith ‘Zaka Zakazi’ amesema: “Tangu mwanzoni mwa msimu huu tuliweka wazi kuwa tuna jambo letu, na hii ni katika kuhakikisha tunajitahidi kumaliza nafasi za juu zaidi kwenye msimamo wa ligi.”
“Hivyo hatuna presha na mtu aliye nyuma yetu, bali sisi tunamwangalia aliye juu yetu, na kwa sasa Young Africans ndiyo vinara wa msimamo wa ligi, hivyo malengo yetu ni kujitahidi kushinda michezo iliyo mbele yetu ili kupunguza pengo la pointi lililo kati yetu.”
“Uzuri ni kwamba Young Africans nao hawajawa na mwendelezo mzuri na wameangusha pointi nyingi, hivyo ni jukumu letu kulichukulia hilo kama faida na kuwakaribia au hata kuwazidi.”