Ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Ihefu FC, umeiwezesha Azam FC kuifikia rekodi waliyoiweka msimu wa 2010/11, ambapo walishinda michezo saba mfululizo ya awali na kufikisha alama 21.
Azam FC jana Jumanne Oktoba 20 ilicheza mchezo wa saba wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku ikiziacha Simba SC na Young Africans zikiwa zimecheza michezo mitano tangu msimu huu 2020/21 ulipoanza.
Azam FC ilianza ligi msimu huu kwa kuifunga Polisi Tanzania bao moja kwa sifuri, kisha ikaichapa Coastal Union mabao mawili kwa sifuri, ikaifunga Mbeya City bao moja kwa sifuri, ikaibamiza Prisons bao moja kwa sifuri, ikainyuka Kagera Sugar mabao manne kwa mawili na kuiadhibu Mwadui mabao matatu kwa moja kabla ya jana kuifunga Ihefu FC mabao mawili kwa sifuri.
Tangu mwaka 2010, Azam FC haijawahi kupata ushindi mfululizo katika michezo saba mfululizo ya mwanzo ya Ligi Kuu, hivyo msimu huu wameifikia rekodi hiyo kwa mara ya kwanza.
Katika msimu wa 2012/2013 timu hiyo ilipata ushindi wa michezo mitano na sare mbili katika michezo saba ilizochezwa mwanzoni mwa Ligi wakati ule wa 2013/2014 ilishinda michezo miwili na kutoka sare michezo mitano, huku msimu wa 2014/2015 ilishinda michezo minne, ilipoteza miwili na sare moja.
Katika msimu wa 2015/2016, Azam ilicheza michezo saba mwanzoni mwa Ligi na kushinda sita huku ikitoka sare mchezo mmoja, wakati msimu wa 2016/2017 ilishinda michezo mitatu, ilitoka sare michezo miwili na kupoteza miwili huku msimu wa 2017/18 katika michezo saba ilishinda mitatu na kutoka sare michezo minne.
Msimu wa 2018/2019, timu hiyo ilipata ushindi katika michezo mitatu na kutoka sare michezo minne katika michezo saba ilizocheza wakati msimu uliopita timu hiyo ilianza ligi na katika michezo saba ya mwanzo ilishinda minne, ilipoteza miwili na kutoka sare mchezo mmoja.