Uongozi wa Azam FC umetangaza donge nono kwa Wachezaji wanaounda kikosi cha klabu hiyo, endapo watafanikiwa kuifunga Simba SC na kutonga Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC msimu huu 2022/23.
Azam FC itapapatuana na Simba SC Jumapili (Mei 07) katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, ukiwa mchezo wa kwanza wa Nusu Fainali ya ASFC, huku mchezo mwingine wa hatua hiyo kati ya Young Africans dhidi ya Singida Big Stars ukitarajiwa kupangiwa tarehe nyingine baada ya kuahirishwa.
Taarifa kutoka ndani ya Azam FC, zimeeleza kuwa, dau ambalo wamewekewa Wachezaji wa wanaounda kikosi cha klabu hiyo ikiwa ni pamoja na Prince Dube na Idris Mbombo ni mkwanja wa maana.
“Mabosi Azam FC hawana utani wanahitaji kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’, wakianza na mchezo wao wa Nusu Fainali dhidi ya Simba SC, wameweka dau nono ambalo litaongeza nguvu kwa wachezaji kusaka ushindi.”
“Ni haki yao wachezaji kucheza kwa kuwa wanatimiza majukumu yao, lakini kuna posho ambazo huwa wanapewa kila mechi wanayocheza na huwa inakuwa hivyo wakishinda,” amesema mtoa taarifa hizi
Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulakarim Amin ‘Popat’ amesema: “Bonasi ipo kila mechi, ikiwemo hizi dhidi ya Simba SC na Young Africans.”
Msimu huu 2022/23 Azam FC imefanikiwa kuifunga Simba SC 1-0 katika mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku ikiambulia sare ya 1-1 kwenye mchezo wa Mzunguuko wa Pili.
Msimu wa 2020/21 timu hizo zilikutana katika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania Bara ‘ASFC’ mkoani Ruvuma kwenye Uwanja wa CCM Majimaji, na Simba Simba SC ilipata ushindi wa 1-0, bao likifungwa na Jose Luis Miquissone.