Kikosi cha Azam FC kimeelekea jijini Dodoma tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa 22 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Dodoma Jiji FC.
Mchezo huo utapigwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kesho Jumamosi (Februari 04) majira ya saa 2:30, ambao unachukuliwa kama sehemu ya kisasi kwa wenyeji Dodoma Jiji FC.
Miamba hiyo ilikutana mwishoni mwa juma lililopita katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam, katika mchezo wa Hatua ya 32 Bora, Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Mchezo huo ulimalizika vibaya kwa Dodoma Jiji FC iliyokubali kufungwa 4-1 na kutupwa nje ya Michuano ya ‘ASFC’, hali ambayo inatazamwa kama mtihani kwao wa kulipa kisasi dhidi ya Azam FC.
Wachezaji waliosafiri kuelekea jijini Dodoma kwa ndege ya Shirika la Tanzania (ATCL) mapema leo Ijumaa (Februari), ni Ali Ahamada, Iddrisu Abdulai, Zuberi Foba, Nathan Chilambo, Edward Manyama, Bruce Kangwa, Malickou Ndoye, Abdallah Kheri, Daniel Amoah, Isah Ndala, Sospeter Bajana, James Akaminko, Kenneth Muguna.
Wengine ni Cleophace Mkandala, Idd Nado, Tepsie Evance, Abdul Sopu, Kipre Junior, Ayoub Lyanga, David Chiwalanga, Yahya Zayd, Idris Mbombo, Prince Dube na Cyprian Kachwele.