Mkuu wa Idara ya Habari na Mwasiliano ya Azam FC Thabit Zakaria ‘Zaka Za Kazi’ ametamba kikosi chao kina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Mapinduzi 2022, licha ya kukutana na Mabingwa wa Tanzania Bara Simba SC.
Azam FC ndio klabu yenye historia ya kutwaa ubingwa wa Mapinduzi mara nyingi zaidi kuliko klabu zote zilizowahi kushiriki michuano hiyo, huku mara ya mwisho kufanya hivyo ilikua mwaka 2020 kwa kuifunga Simba SC bao moja kwa sifuri.
‘Zaka Za Kazi’ amesema kikosi chao kina asilimia kubwa ya kuibuka Mabingwa wa Michuano hiyo mwaka huu kwa sababu kimetinga hatua ya fainali kwa kishindo kikubwa kwa kuifunga Young Africans iliyokua Bingwa Mtetezi.
Amesema mbali na kuifunga Young Africans safari yao ya kusaka taji la Mapinduzi 2022, ilikua ya kishindo kwa kuifunga Meli 4 City bao 1-0, Yoso Boys mabao 5-1 na Namungo FC bao 1-0.
“Sisi ndio wenye asilimia kubwa ya kutwaa ubingwa huu kwa sababu tumeingia Fainali kwa kishindo tumempiga mtu goli mbili tukampiga tena mtu goli Tano tukamaliza na wale jamaa tukawapiga goli tisa.” amesema ‘Zaka za kazi’
Azam FC imetwaa Kombe la Mapinduzi mara tano (2012, 2013, 2017, 2018 na 2019) huku Simba SC ikitaa ubingwa wa michuano hiyo mara mbili (2011 na 2015).