Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imetangaza kuwa nchi za Azerbaijan na Armenia zimeafikiana kusitisha mapigano kuanzia saa sita Jumamosi katika jimbo lililojitenga la Nagorno-Karabakh, baada ya mazungumzo kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa hayo mawili huko Moscow.
Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema makubaliano hayo ya kusitishwa mapigano yatawezesha nchi hizo mbili kubadilishana wafungwa wa kivita na miili ya waliouawa kulingana na vigezo vya Kamati ya Msalaba Mwekundu
Tangazo hilo linatolewa baada ya masaa 10 ya mazungumzo ya kidiplomasia yaliofanyika nchini Urusi, ambayo yaliratibiwa na Waziri wa Mambo ya Nje ya Urusi, Sergey Lavrov.
Lavrov amesema hatua hiyo ya kusitishia mapigano itafungua njia ya mazungumzo ya kusuluhisha mgogoro huo.
Mapigano hayo ya sasa kati ya Azerbaijan na Armenia, ambayo yalianza Septemba 27 na kusababisha vifo vya mamia ya watu yanahusisha mzozo wa miongo kadhaa kuhusu jimbo la Nagorno-Karabakh ambalo kiasili ni sehemu ya Azerbaijan lakini limekuwa katika udhibiti ya jamii ya wachache ya Waarmenia, tangu kumalizika kwa mapigano ya kujitenga ya 1994.
Kwa karibu wiki mbili kumekuwa na mapigano mapya na makali huko Nagorno-Karabakh, ambapo mamia ya watu wameuawa.