Ikiwa Leo Oktoba 10 Dunia inaadhimisha siku ya Afya ya akili, Idadi ya wagonjwa wa akili nchini imeongezeka kutoka 29,166 mwaka 2018/19 hadi 33,287 mwaka 2019/20 huku wanaume wakitajwa kuathirika zaidi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kati ya wagonjwa hao idadi ya wanaume ilikuwa 18,535 kulinganisha na wanawake ambao walikuwa 10,631 kwa mwaka 2018/19.

Idadi hiyo ni wale waliotibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Mloganzila, jijini Dar es Salaam.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Afya ya Akili MNH, Dkt. Fileuka Ngakongwa amesema sababu za wanaume wengi kuugua matatizo ya akili katika umri mdogo ni kutokana na msongo wa mawazo, ugumu wa maisha na kuweka vitu moyoni kulinganisha na wanawake ambao huzungumza.

Sababu nyingine zilizotajwa ni mazingira wanayoishi watu, mazingira ya kazi, kukosa amani, vinasaba vya akili na magonjwa ya mwili kama Malaria, Homa ya Kichwa na Uti wa Mgongo, ajali ya kichwa, maambuzi ya UKIMWI kwenda kichwani na magonjwa yasiyoambukiza.

Dkt. Fileuka ametaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni kukosa usingizi, unywaji wa pombe kupita kiasi, woga uliopitiliza, mtoto kukojoa kitandani katika umri ambao alishapita hatua hiyo.

Oktoba 10 kila mwaka dunia inaadhimisha siku ya afya ya akili ambapo takwimu zinaonesha kuwa takribani watu bilioni 1 duniani kote wanaishi na matatizo ya akili.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake kwa siku hii amesema, inabidi hatua zichukuliwe ili kuhakikisha kunakuwa na huduma bora ya afya ya akili kwa wote kwani hivi sasa inaonesha pia kuwa kila sekunde 30 mtu mmoja anajiua kutokana na tatizo hili la afya ya akili. 

Covid 19 Ulaya bado kizungumkuti
Wizara ya maji yaagiza Bukoba mjini kufikishiwa maji kwa asilimia 100