Mbunge wa Geita Vijijini kwa tiketi ya CCM, Joseph Kasheku maarufu kama Msukuma aliwashangaza wengi baada ya kutoa hoja Bungeni akitaka madawa ya kulevya aina ya Bangi na Mirungi ihalalishwe kwa madai kuwa ina faida kiuchumi na kiafya.

Msukuma aliitaka Serikali kufanya utafiti mwingine ili kubaini tena faida na hasara ya zao hilo haramu kwani anaamini lina faida zaidi ukilinganisha na viroba ambavyo vimeruhusiwa.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla ambaye kitaaluma ni Daktari alieleza kuwa Bangi ina madhara makubwa sana hususan kiakili. Hivyo, Serikali haiwezi kuihalalisha wala kujadili suala hilo.

Katika hatua nyingine, Mwanaharakati Malisa Godlisteni alimtafuta Daktari aliyebobea katika masuala ya madawa ya binadamu, Dk. Christopher Cyrilo na kumuomba aeleza kama kuna faida yoyote kiafya kwa kutumia mmea wa bangi na sababu zilizosababisha baadhi ya nchi kuiruhusu.

Pamoja na kueleza kuwa kuna hasara kubwa ya kisaikolojia au kiakili, Dk. Cyrilo alieleza pia faida ya kiafya inayotokana na matumizi ya bangi huku akionya kuwa matumizi hayo katika nchi zilizoruhusu, ni lazima yawe yamependekezwa na Daktari baada ya kumchunguza mhusika na kubaini tatizo lake na sio vinginevyo.

Hivi ndivyo alivyoeleza kwa maandishi Dk. Christopher Cyrilo: 

Katika baadhi ya nchi Duniani, matumizi ya bangi yamehalalishwa kuzingatia utashi wa mamlaka za nchi husika. Uruguy na Marekani (katika majimbo 20) ni mifano ya nchi hizo. Tafiti mbalimbali za kiafya zimefanyika na kupelekea ugunduzi kuwa bangi huweza kutumika kama tiba kwa baadhi ya magonjwa, isipokuwa haipaswi kutumika ovyo kama ilivyo kwa dawa zingine.

Zifuatazo ni faida 11 za kiafya za bangi. Kisha tutaeleza na athari hasi za bangi hapo baadae.

1. Inaweza kutumika kukinga na kutibu presha ya jicho (glaucoma), bangi inapunguza presha ya jicho (intraocular pressure) kwa watu wenye presha ya kawaida na hata wale ambao presha ya jicho iko juu( glaucoma).

2. Inaweza kuboresha afya ya mapafu na kupunguza athari za tumbaku katika mapafu. Januari 2012, tafiti zilionesha bangi haiathiri kazi za mapafu badala yake huongeza ufanisi wa mapafu.

3. Huweza kuzuia kifafa. Kemikali aina ya “Tetrahydrocannabinol” au “THC” iliyopo katika bangi huambatana na seli za ubongo zinazochochea umeme katika mfumo wa fahamu. Muambatano huo hupunguza msisimko (excitability) wa mfumo wa fahamu na kuzuia kutokea kwa kifafa.

4. Kuzuia kuenea kwa baadhi ya kansa, “Cannabidiol au CBD” ni kemikali iliyopo kwenye bangi ambayo hupunguza kuenea kwa kansa mwilini. Mfano, kansa ya matiti.

5. Inapunguza wasiwasi, maumivu na kichefuchefu, hata hivyo ikitumiwa kwa kiasi kikubwa huweza kuongeza wasiwasi.

6. Hupunguza na kutibu matatizo ya kutetemeka kwa misuli, (Parkinsonism)

7. Bangi huweza kutibu magonjwa ya utumbo (Inflammatory bowel diseases). Mwaka 2010 katika chuo cha Nottingham, tafiti ziligundua kuwa kemikali zilizopo kwenye bangi husaidiana na seli za mwilini kuongeza kinga za mwili na ufanisi wa utumbo.

8. Kupunguza maumivu ya viungo. Bangi hupunguza maumivu, hupunguza miwasho na kuleta usingizi.

9. Huboresha ngozi na kuchangamsha kazi za mwilini, Pia huongeza matumizi ya sukari mwilini.

10. Huongeza uwezo wa kubuni vitu (creativity), uwezo wa kukumbuka na uwezo wa kuzungumza.

11. Huweza kusaidia watu wanaopata matatizo ya mfadhaiko kutokana na kumbukumbu za mambo ya kutisha (post traumatic stress disorder) Mfano, Kwa wahanga wa majanga ya asili na yale yasio ya asili kama vita, moto, tsunami nk. Watu hao hupata kuona upya matukio ya kutisha walioshuhudia zamani na huweza pia kuyaona katika ndoto. Bangi huweza kuwasaidia kuepuka tatizo hilo. Maveterani wa vita ni mfano mzuri kabisa.

ANGALIZO. Matumizi ya kiafya ya bangi yanapaswa kuwa chini ya maelekezo ya daktari au mtaalamu wa afya, kwa sababu athari zake hutegemea kiasi cha matumizi na hali ya afya ya mtumiaji. Inaaminika kuwa Bangi ina athari chache kulinganisha na pombe.

Asante.

Bakwata yabariki Marudio ya Uchaguzi Zanzibar
Polisi watoa tamko kuhusu maandamano ya vijana wa Chadema kwenda Ikulu Kesho