Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuhakikisha linakuwa na nidhamu katika utendaji wake, ili kupunguza lawama zinazotolewa na baadhi ya watu juu ya Askari wake wachache wasio waadilifu.
Kitwanga ameyasema hayo, katika mahojiano maalumu na Dar24 Media nyumbani kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni na kusema lawama nyingi zimekuwa zikitolewa kwa Jeshi hilo, kutokana na baadhi ya matendo yasiyokuwa na uadilifu ambayo hayana ulazima.
Amesema, “lawama kwa jeshi la Polisi zinatolewa na watanzania ambao wanahudumiwa na Polisi, na ukiwalaumu polisi moja kwa moja unakosea maana wao ndiyo wanao wahudumia wananchi kinachotakiwa ni kitu kimoja tu, wajitambue.”
Kitwanga amezidi kueleza kuwa, “Nasisi Watanzania tuwe waadilifu tumtangulize Mungu mbele, sikatai wapo askari ambao nidhamu yao si nzuri sana na anaweza akafanya makosa, chukua makosa yote ya waliokuwepo mahabusu au waliofungwa angalia asilimia ngapi wamebambikiziwa makosa si yao?.”
Aidha, ameongeza kuwa ipo haja ya askari Polisi kuishi kambini, ili kuwarahisishia kufanya kazi kwa wakati hasa inapotokea dharura huku akisema, “Polisi ni jeshi, kama askari mmoja anakaa Gongolamboto, mwingine sinza, ikitokea dharura hawa watakusanyika saa ngapi?.’’
Katika hatua nyingine, Kitwanga amesema, aliwahi kusema katika ufunguzi wa nyumba za Askari eneo la barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam kuwa ni muhimu kuendeleza ujenzi wa yumba hizo kwa manufaa ya nchi.
Ameongeza kuwa, “Serikali ina wabia ni kuangalia kipaumbele je tukope tujenge nyumba za askari au tujenge madara au tujenge barabara vyote ni muhimu kama tunadhani usalama wa raia ni lazima kwanini tusiweke nguvu za kujenga hizo nyumba.”
Hata hivyo, ameeleza jinsi alivyokuwa na dhamira ya kuweka kamera katika baadhi ya maeneo ‘smart city’ lengo likiwa ni kuboresha zaidi ulinzi na kupunguza matumizi ya rasilimali watu katika maeneo yasiyo na ulazima wa kuwa na Askari wengi wanaolinda majengo au taasisi kama Benki.
“Wakati ule tunajenga zile nyumba za kilwa road na nililisema kipindi kile wakati tunafungua zile nyumba kwamba ni muhimu hili likawa ni la kuendeleza na jingine amablo nilitamani sana kuwa na Camera kila maeneo hii inaitwa smart city.” amefafanua Kitwanga.