Aliyewahi kuwa Kiungo Klabu Bingwa Tanzania Tanzania Bara Young Africans na Taifa Stars, Abdi Kassim ‘Babi’ amesema kutokana na ubora wa timu hiyo anaipa nafasi kubwa ya kushinda mechi yao ya kwanza ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Marumo Gallants.

Mechi hiyo imepangwa kuchezwa leo Jumatano (Mei 10) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kuanzia saa 10:00 jioni, ambapo Young Africans walitinga hatua hiyo baada ya kuitoa Rivers United ya Nigeria kwa jumla ya mabao 2-0, hatua ya Robo Fainali.

Babi amesema anaipa nafasi kubwa ya kushinda kutokana na ubora wa kikosi walichonacho sasa na kwamba kikubwa wachezaji wanatakiwa kutambua kuwa wapo nyumbani na wamebeba jukumu la kuwafurahisha mashabiki wao pia kuweka rekodi mpya ya kwenda fainali kwa mara ya kwanza.

“Young Africans wamebadilika sana kuanzia benchi la ufundi na wachezaji walionao kwangu mimi naiona ikitoboa na kwenda fainali lakini lazima wapambane.” amesema Babi

Amesema timu hiyo haijafika Nusu Fainali kwa kubahatisha bali kwa juhudi za wachezaji, benchi ya ufundi ambayo inachagizwa na uwekezaji mkubwa waliofanya.

Baada ya mchezo huo, Young Africans itasafiri kwenda Afrika Kusini kucheza mchezo wa marudiano Mei 17, ambao unatarajiwa kuamua hatima ya mabingwa hao watetezi katika mashindano hayo ya pili kwa ukubwa ngazi ya klabu Barani Afrika.

Dube achekelea kuzifunga Simba, Young Africans
Mwingine aokolewa shambani kwa mchungaji Mackenzie