Uongozi wa Leeds United unajiandaa kuzungumza na Meneja wa zamani wa Crystal Palace, Patrick Vieira ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi kwenye benchi la ufundi la miamba hiyo ya Elland Road.
Vieira mwenye umri wa miaka 46, alifutwa kazi na Palace Machi mwaka huu baada ya kushindwa kushinda mchezo wowote kwa mwaka 2023 na amekuwa hana kazi tangu muda huo.
Kwa sasa gwiji huyo wa Arsenal ni mmoja kati ya makocha watatu wanapigiwa hesabu na mabosi wa Elland Road ili wakapige kazi kwenye timu hiyo, huku wengine ni Scott Parker na kocha wa zamani wa Norwich, Daniel Farke.
Mazungumzo yanaendelea na Meneja wa West Brom, Carlos Corberan, aliyewahi kuinoa Leeds, lakini timu hiyo iliyoshika daraja mwaka huu inafikiria kuachana na mpango wa kumchukua Mhispania huyo licha ya kukubalika na mashabiki.
Corberan alifanyakazi chini ya Marcelo Bielsa alipokuwa akisimamia kikosi cha chini cha miaka 23.
Leeds wanataka kocha ambaye hana mkataba na timu nyingine ili kukwepa kulipa fidia. Licha ya kushuka daraja na kucheza Championship msimu ujao, Leeds wanataka kuteua kocha mwenye uzoefu wa Ligi Kuu England.
Leeds ilitaka kuzungumza na Meneja wa zamani wa Leicester City, Brendan Rodgers, lakini ameshachukuliwa na Celtic ya Scotland.
Meneja wa zamani wa Bournemouth na Fulham, Parker, ambaye mara mbili amezipandisha daraja timu kutoka kwenye Championship, naye alikuwa anafukuziwa na mabosi wa Leicester City.
Lakini, miamba hiyo ya King Power imemteua Enzo Maresca na kumpa mkataba wa miaka mitatu baada ya kuwa msaidizi wa Pep Guardiola huko Manchester City.