Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Mkoa wa Katavi Sheikh Mashaka Kakulukulu amewaomba Wadau wa maendeleo kuchangia ujenzi wa Zahanati ya Mama na Mtoto, unaotarajiwa kufanyika katika eneo la mtaa wa Tulieni uliopo nje kidogo ya mji wa Mpanda.

Akiwa ameongozana na baadhi na Viongozi wa Jumuiya za BAKWATA Mkoani, Sheikh Kakukulu ameitaka Jumuiya ya Wanawake wa Kiisalamu – JUWAKITA, Mkoa wa Katavi ambayo ndio msimamizi wa mradi huo, kuhahakisha kazi ya ujenzi wa kituo hicho inaanza mara moja.

Amesema, mradi huo unapaswa kuanza kwa namna yoyote hata kwa rasilimali chache zilizopo, ili kuweza kuwatia moyo waumini wengine ambao watawiwa kuchangia ujenzi huo.

“Mwenyezi Mungu amemwambia Mtume Muhammad (S.A.W) lakini anatuambia sote kwamba fanyeni, tendeni Mwenyezi Mungu ataoana vile mnachofanya lakini pia Mtume (S.A.W) ataona mnachofanya na waumini pia wataona, kwahiyo sisi tukianza wapo waja wa Allah atawaleta watakuja kufanya jambo hili na jambo hili litakuwa jepesi,” alisema Sheikh Kakulukulu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa JUWAKITA Mkoa wa Katavi, Rehema Kamasesela amesema tayari eneo hilo limeshapimwa na wamepeleke zaidi ya tofali 2500 kwa ajili ya kuhakikisha mradi huo unaanza mara moja, huku akiwaomba Wanawake wa Kiislamu kufikisha ujumbe kwa waumini wengine kwa ajili ya kusaidia ujenzi huo.

Amesema, “JUWAKITA ni wasimamizi tu, lakini kujenga sisi peke yetu hatuwezi ndio maana tumewaita, hivyo naomba mkatutangazie kwa waumini wote, ndugu zetu, majirani, rafiki zetu wa mkoa huu na hata nje ya mkoa na nje ya nchi ili kufikia mwezi wa 12 Mwenyezi Mungu akipenda Inshaalla alama iwe imeonekana.”

Zahanati hiyo ya Mama na Mtoto ni moja kati ya miradi kadhaa inayotekelezwa na Baraza kuu la Waislamu – BAKWATA, Mkoa wa Katavi katika Wilaya zote, ambapo miradi mingine ni ujenzi wa Shule ya msingi ya Mufti Aboubakary Bin Zubeir, Ofisi za BAKWATA kwa kila Wilaya na Ujenzi wa Misikiti mipya ya kisasa inayoambatanishwa na shule za Madrasa.

Sekta ya Madini chachu ya maendeleo - Dkt. Biteko
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Novemba 12, 2023